✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 11: Kisasi cha Damu

Giza la usiku lilitanda nje ya jengo la LEGO, lakini moyo wangu ulikuwa unawaka moto wa hasira na hofu. Nikiwa nimejificha nyuma ya kontena kuu la mizigo pamoja na Mzee Yusufu, niliishika ile bastola kwa mikono inayotetemeka. Hii haikuwa tena hadithi ya kitandani na Katherini; huu ulikuwa ni ukweli mchungu wa maisha na kifo.

Ghafla, taa za gari kubwa la kifahari zilipasua giza. Danieli alishuka, uso wake ukiwa umekunjamana kama karatasi iliyowekwa maji. Nyuma yake walitoka wanaume wawili wenye miili iliyojengeka, wakimvuta mtu aliyekuwa amefungwa kamba mikononi na gunia kichwani.

Walipomfanya apige magoti kwenye sakafu ya zege na kumvua lile gunia, nilijikuta nikiziba mdomo kuzuia kelele. Alikuwa ni Katherini. Uso wake ulikuwa umevimba na damu ilikuwa ikimtoka puani.

"Niambie Aroni yuko wapi!" Danieli alinguruma, akimshika Katherini nywele na kumuuliza kwa sauti ya kikatili. "Najua ulikuwa unajua kila kitu tangu mwanzo. Ulilala naye, ulimhisi, na sasa unataka kumficha? Mimba ilikuwa ya nani ikiwa Aroni ndiye aliyekuwa anamiliki kitanda chako?"

Katherini alitema damu chini na kucheka kicheko cha kinyonge. "Baba... hata ukiniua, Aroni ameshatuponoka. Desderia amekufa, na sasa unakwenda kukutana na kivuli cha mtu uliyemuua miaka iliyopita."

Danieli alipandwa na wazimu. Alichomoa bunduki yake na kuiweka kwenye paji la uso la binti yake mwenyewe. "Unadhani nitasita kukuua? Kama nilivyowamaliza wazazi wa Aroni ndani ya gari lao bila kupepesa macho, wewe ni nani kwangu ikiwa unataka kunizuia kuwa mfalme wa LEGO?"

Kauli ile ilitosha. Yale yalikuwa ni maungamo niliyokuwa nayasubiri maisha yangu yote. Alikuwa ni yeye. Danieli, mtu niliyemuita "Baba," ndiye aliyeyakatisha maisha ya wazazi wangu.

"Sasa hivi, mwanangu," Mzee Yusufu alinong'ona pembeni yangu. "Huu ndio wakati wa Aroni kusimama."

Nilitoka kwenye giza, bastola yangu ikiwa imenyooka mbele. Sauti yangu haikuwa tena ile ya Desderia mnyonge, bali ilikuwa sauti nzito iliyojaa mamlaka na kisasi. "Mueke chini Katherini, Danieli! Leo ndio siku ya hesabu!"

---

**Kionjo cha Sehemu ya 12:**
*Danieli alishtuka na kugeuka, akinitazama kwa mshangao mkuu anapoona sura ya Desderia lakini akiwa na sauti na ujasiri wa Aroni. "Wewe?!" alipayuka huku akijaribu kufyatua risasi. Wakati huo huo, ving'ora vya polisi vilianza kusikika kwa mbali, lakini Remi alitokea upande wa nyuma akiwa na kisu akielekea shingoni mwa Mzee Yusufu...*

**ITAENDELEA SEHEMU YA 12: MWISHO WA USALITI**