✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 18: KIMBUNGA NYUMBANI

Kikao cha kanisa kiliisha kwa maombi ya toba na shukrani, huku wazee wakiamini kabisa kuwa Shetani alijaribu kuivuruga ripoti ya Mchungaji. Lakini kwangu, hali haikuwa ya amani hata kidogo. Safari ya kurudi nyumbani ilikuwa kama kuelekea kwenye hukumu ya kifo.

Mama alikuwa akitembea mbele yangu kwa mwendo wa kasi, joho lake likipeperuka kwa upepo wa jioni. Hakunigeukia hata mara moja, na ukimya wake ulikuwa unatisha kuliko kelele za Mzee. Nilijua fika kuwa ameniokoa kanisani ili kulinda heshima ya familia na jina lake kama katibu, lakini nyumbani mambo yangekuwa tofauti.

Tuliingia getini, tukamkuta Mzee ameketi barazani akisoma gazeti la jioni huku akinywa chai. Alipotuona tu, aliweka gazeti chini na kutoa miwani yake.

*"Ehee, Mama Neema! Mbona mmerudi mapema hivyo? Na huyu kijana mbona ameloa jasho na vumbi namna hiyo? Kwani kikao kimeendaje?"* Mzee aliuliza kwa sauti ya udadisi.

Mama alisimama katikati ya uwanja, akamtazama Mzee, kisha akanitazama mimi. Mapigo ya moyo wangu yalikuwa yanasikika mpaka kooni. Niliishika ile rula niliyodai naitafuta asubuhi kama kingao changu cha mwisho.

*"Baba Neema,"* Mama alianza kwa sauti ya upole lakini iliyojaa uzito. *"Kikao kimeenda salama, lakini kuna jambo limetokea kule kanisani ambalo lazima tulijadili hapa hapa kabla giza halijaingia."*

Mzee alikunja uso, akajua kuna jambo zito. *"Jambo gani hilo? Kuna mtu amekosea mahesabu ya michango?"*

Mama alinitazama kwa jicho la ukali. *"Mwanangu, ingia ndani sasa hivi. Nenda kamsubiri Baba yako sebuleni. Na usithubutu kutoka mpaka nikuite."*

Niliingia ndani huku nikichechemea kidogo ili kuendeleza ule uongo wa "kuumia mguu," lakini Mama alinisukuma kwa hasira. *"Acha maigizo! Ingia ndani!"*

Niliketi sebuleni, nikiwasikiliza kupitia dirisha la kioo. Mama alianza kuelezea kila kitu kilichotokea kanisani—ile picha ya "warumi" iliyotokea kwenye ukuta, fujo zilizotokea, na jinsi nilivyovunja deki ya kanisa. Lakini alifanya jambo moja ambalo sikulitegemea; hakusema kuwa ile CD ilikuwa yangu tangu mwanzo. Alisema fundi ndiye aliyefanya makosa makubwa ya kuchanganya vitu vya ajabu kwenye ripoti ya Mchungaji.

Lakini Mzee siyo mtu wa kudanganywa kirahisi. Alisimama kwa ghafla, akagonga meza ya chai.

*"Fundi mkuu? Fundi mkuu namjua tangu ujana wangu, hajawahi kuwa na uchafu huo! Hapa kuna mchezo mchefu umefanyika,"* Mzee alinguruma. *"Na huyu kijana aliyekuwa anahangaika na deki tangu jana usiku ndiye anajua ukweli!"*

Mzee aliingia ndani kwa kishindo, macho yake yakiwa yamejaa hasira. Alielekea moja kwa moja kwenye deki yetu ya sebuleni iliyokuwa imetulia pale.

*"Kijana! Njoo hapa!"* Mzee aliita. *"Fundi amesema deki hii haina shida. Nataka uwashe sasa hivi, na kama nikikuta hata harufu ya uongo wako humu ndani, leo utajua kwanini naitwa baba yako!"*

Nilihisi miguu inalegea. Deki sasa hivi ilikuwa na CD ya kwaya niliyoiweka usiku wa manane. Lakini sikuwa na uhakika kama nilifunga skrubu vizuri au kama kuna alama yoyote niliyoiacha wakati naifungua kwa kisu cha jikoni.

Mzee alichukua rimoti na kunikabidhi. *"Washa! Nataka nione kile fundi alichokiona!"*

**ITAENDELEA...**

---
**Episode 19 Inakuja: "MTIHANI WA MWISHO WA DEKI"**