โœฆ Matangazo โœฆ

๐Ÿ“– Story Tamu

Episode 5: MSHTUKO MLANGONI: MGENI ASIYEKARIBISHWA

*(Sauti ya mvua nyepesi inaanza kunyesha, ikigonga mapaa ya bati ya vibanda vya mtaani. Katika geti kubwa la rangi ya kijivu la nyumba ya binti, taa za usalama zinangโ€™ara kwa mbali.)*

Binti alikuwa amekaa sebuleni akijaribu kutulia, lakini kila sauti ya gari iliyopita nje ilimfanya ashtuke. Alikuwa amepanga kuwaweka mama yake na yule jirani kwenye nyumba ya wageni, lakini jirani huyo, kwa kuona hali ya mama inazidi kuwa mbaya na akiwa hana pesa ya kutosha, aliamua kutumia anwani aliyoijua tangu zamani kufika moja kwa moja nyumbani kwa binti.

*(Sauti ya honi ya teksi ikilia nje ya geti: "Piii! Piii!")*

Moyo wa binti ulilipuka. Alikimbia dirishani na kuchungulia kupitia pazia zito la hariri. Alimuona yule kijana jirani akimshusha mama yake kwny teksi iliyochakaa. Mama alikuwa amejifunga khanga kichwani, akionekana mnyonge na mwenye baridi.

"Mungu wangu! Wamefikaje hapa?" alijisemea binti kwa sauti ya kukata tamaa.

Alitoka nje kwa kasi kabla mlinzi hajafungua geti. Alipofika nje, badala ya kumkumbatia mama yake, macho yake yalikuwa yamejaa hasira na hofu ya kuonekana na majirani.

"Mlifuata nini hapa? Niliwaambia nini kwenye simu?" binti alifoka kwa sauti ya chini lakini iliyojaa sumu.

Mama yake, akizani labda mwanae anatania, alijaribu kusogea amkumbatie huku akitabasamu kwa unyonge. "Mwanangu... nimefika. Nilikuwa nakuota kila siku..."

Binti alirudi nyuma hatua mbili, akiepuka mikono ya mama yake iliyokuwa na vumbi la safari. "Mama, huwezi kuingia humu! Hii nyumba ni ya kampuni, na sheria ni kali sana. Haruhusiwi mtu yeyote kukaa hapa!"

Mama aliganda. Machozi yalianza kumlengalenga. "Mwanangu, mimi ni mama yako... hata kukaa sebuleni tu nipumzishe miguu?"

"Hapana! Nimesema hapana!" binti alimgeukia yule jirani kwa ukali, "Mchukue, mpeleke hapa jirani kuna gesti. Kesho asubuhi nitakuja kuwapa hela ya kurudi kijijini. Sitaki mazoea haya!"

*(Sauti ya radi ikinguruma kwa mbali, ikifuatiwa na sauti ya mama akivuta pumzi kwa uchungu, akitazama nyumba ya kifahari ya mwanae ambayo kwake ilikuwa kama gereza lisilo na huruma.)*

Binti aligeuka na kuingia ndani, akifunga geti kwa kishindo kikubwa, akimwacha mama yake amesimama kwenye mvua inayozidi kuongezeka, akiwa ameshika fundo lake la nguo na mfuko wa karanga uliokuwa umeanza kulowa.

---
**ITAENDELEA SEHEMU YA 6...**