✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 14: Usaliti Katikati ya Giza

Usiku ule Happy hakulala. Kila akifumba macho, aliona ile milioni moja ikicheza mbele yake, na kila akifumbua, aliona kile kifaa kidogo cha kunasa sauti kikiwa kimefichwa ndani ya sidiria yake. Hofu na tamaa zilikuwa zikipigana mieleka kifuani mwake. "Asha ashanitupa, Saidi ananitumikisha... kwanini niteseke?" alijisemea akijipa ujasiri wa uongo.

Siku iliyofuata, Happy alifika kazini akiwa amepooza. Alifanya kazi zake kwa unyonge kuliko kawaida, akingojea saa ya watu kuondoka ifike. Saa kumi na moja jioni ilipotimia, ofisi zilianza kuwa tupu. Asha alipita kumuaga, "Happy, mimi nawahi kidogo, leo tuna kikao cha nje na Boss. Utamaliza salama?"

Happy aliitikia kwa kichwa tu, huku moyo ukimvuta kumwambia Asha kila kitu, lakini kivuli cha milioni moja kikamziba mdomo.

Baada ya nusu saa, Happy alibaki peke yake kwenye korido ya ghorofa ya juu. Alishika dekio lake na kuelekea ofisi ya Saidi. Kwa kawaida, alikuwa na ufunguo wa akiba kwa ajili ya usafi. Alifungua mlango taratibu, giza la ofisi ile likamkaribisha. Aliingia ndani, akasogea mpaka kwenye meza kubwa ya Saidi.

Alipiga magoti na kuanza kukipachika kile kifaa chini ya meza. Mikono ilikuwa ikimvuta jasho jingi. "Nishamaliza," alinong'ona baada ya kusikia sauti ya 'click' ikionyesha kifaa kimekaa.

Alipoinuka tu ili atoke, ghafla taa kubwa za ofisi ziliwaka kwa pamoja. Happy alipiga yowe na kuanguka chini kwa mshtuko.

"Umepoteza nini chini ya meza yangu, Happy?" Sauti ya Saidi ilisikika ikiwa na utulivu wa kutisha.

Happy aligeuka na kumuona Saidi akiwa amesimama mlangoni, huku pembeni yake akiwa na James na Asha. Asha alikuwa akilia, huku akimwangalia Happy kwa masikitiko ambayo Happy hakuwahi kuyaona maishani mwake.

"Boss... mimi... nilikuwa nafuta vumbi..." Happy alijaribu kusema, lakini James alimsogelea na kukivuta kile kifaa kutoka chini ya meza.

"Vifungo vya siku hizi vina uwezo wa kunasa sauti?" James alisema kwa kejeli. "Happy, tulikupa nafasi ya mwisho. Tulijua Pili atakutafuta, na tulijua Manyama atataka kukutumia. Tulikupa mtihani wa uaminifu, na umeufeli ndani ya saa ishirini na nne tu."

Happy alimwangalia Asha kwa macho ya kuomba msaada. "Asha, nisaidie! Walinitishia... Pili aliniambia kama nisipofanya hivi wataniua!"

Asha alijifuta machozi na kusogea mbele. "Uongo Happy! James alikuwa nje ya ile baa jana, amesikia kila kitu. Amesikia jinsi ulivyokuwa na wivu na mimi, amesikia jinsi ulivyokubali kuipokea ile milioni moja kwa furaha. Happy, kumbe hata adhabu ya hotelini haikutosha kukubadilisha?"

Saidi alipiga hatua mbili mbele. "Unajua kwanini sikukupeleka polisi mwanzo? Nilitaka nione kama 'mla nauli' anaweza kuwa mtu mwaminifu akichoka kusugua vyoo. Manyama ni mshindani wangu, na alichotaka kufanya ni kosa la jinai. Na wewe, umekubali kuwa mshiriki wake."

Happy alianguka miguuni mwa Saidi. "Nisamehe Boss! Sitaki kwenda jela! Nitafanya kazi maisha yangu yote bila mshahara, tafadhali!"

Saidi alimtazama James na kutoa ishara ya kichwa. James alitoa pingu. "Safari hii huna dhamana, Happy. Na Pili Kiswaswadu naye anasubiriwa kule kule alikotoka. Manyama ana kinga ya pesa, lakini ninyi vibaraka wake mtakuwa mfano kwa wengine."

Wakati Happy akitolewa nje huku akipiga kelele za kuomba msamaha, Asha alibaki amesimama ofisini humo, akijihisi mpweke zaidi kuliko alivyokuwa mwanzo. Rafiki yake wa utotoni, mshauri wake wa siri, sasa alikuwa anaenda kupotea kabisa.

"Asha," Saidi alimwita kwa sauti ya upole. "Usihuzunike. Kwenye safari ya mafanikio, lazima uwaache nyuma wale wanaotaka kukurudisha kwenye vumbi."

Lakini je, Saidi alikuwa rafiki wa kweli au naye alikuwa anasuka mtego mwingine kwa ajili ya Asha?

---
**ITAENDELEA...**