✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 8: UKWELI KWENYE MEZA

Mapigo ya moyo yalinidunda kwa kasi ya ajabu. Mzee alisimama pale sebuleni kama jaji mkuu, huku marafiki zangu, Juma na mwenzake, wakitetemeka kando ya mlango. Mama naye aliweka fagio chini na kusogea karibu, akitaka kujua ni kitu gani hicho cha ajabu kilichopatikana kwenye deki yetu "takatifu."

Nilihisi kama ardhi inataka kupasuka nimezwe. Mzee aliishusha ile deki juu ya meza kwa kishindo kidogo. *"Fundi ameniambia deki haina shida yoyote ya nyaya kama ulivyodai jana,"* alisema Mzee huku akinitazama kwa jicho la shaka. *"Lakini amesema alipoiwasha tu, alikuta kitu ambacho hakikutarajiwa."*

Juma alinitazama kwa jicho la kuomba msaada. Alijua fika kuwa siri yetu ikivuja, hata yeye atapata matatizo kwao. Nilikumbatia lile daftari la Fizikia nikiwa nimekazana, nikijua ndani yake ndipo palipo na ile CD ya "warumi" niliyokuwa nimeitoa usiku.

*"Fundi amekuta nini mzee mwenzangu?"* Mama aliuliza kwa udadisi, sauti yake ikionyesha wasiwasi.

Mzee alipumua kwa nguvu. *"Amekuta CD ya kwaya ambayo haina hata lebo, na imekwaruzika vibaya mno mpaka inasumbua deki kusoma. Amesema hiyo CD ndiyo iliyokuwa inasababisha deki 'kustack' na kutoa sauti za ajabu jana."*

Nilihisi kama nimepewa uhai mpya! Kumbe ile CD ya kwaya niliyoiingiza usiku wa manane kwa haraka ilikuwa mbovu, na fundi aliamini ndiyo chanzo cha matatizo ya deki. Mzee hakuwa amegundua chochote kuhusu ile CD ya kwanza.

*"Sasa nyinyi vijana, mmekuja kufuata nini hapa asubuhi yote hii?"* Mzee aliwageukia Juma na mwenzake.

Juma, akiona upenyo wa kutokea, alijibu haraka: *"Mzee, tulikuja kufuata ile CD yetu ya kwaya tuliyomuazima rafiki yetu jana asubuhi aifanyie mazoezi. Tulijua labda ndiyo imesababisha matatizo, ndiyo maana tumekuja kuichukua tuipeleke kwa mwenyewe."*

Mzee aliichomoa ile CD ya kwaya mbovu kwenye deki na kuwarushia. *"Chukueni huu uchafu wenu! Na sitaki mwanangu azime tena vitu vibovu hivi, vinaharibu deki yangu!"*

Washikaji waliondoka kwa kasi ya ajabu, huku wakinitolea macho ya *"tutakukoma mbele"*. Nilibaki pale nikiwa nimeshikilia lile daftari langu la Fizikia, nikijua bado nina bomu lingine mkononi—ile CD halisi ya aibu ilikuwa bado imejificha ndani ya kurasa za Fizikia.

Mama alitikisa kichwa. *"Pole sana mwanangu, kumbe ni hiyo CD ya kwaya ndiyo ilikupa homa jana? Haya, nenda kajiandae na tuition."*

Nilirudi chumbani kwangu nikiwa na furaha ya ushindi, lakini furaha hiyo ilikatika ghafla nilipolifungua lile daftari langu la Fizikia ili niichukue ile CD niivunje au niitupe mbali.

Daftari lilikuwa tupu. Ile CD haikuwepo!

Nilikumbuka... asubuhi ile nikiwa bado nimejifunika shuka, mdogo wangu wa kike alikuwa ameingia chumbani kwangu kuchukua 'rula' kwa ajili ya tuition. Je, inawezekana aliona ile CD na kuichukua akidhani ni ya katuni?

**ITAENDELEA...**

---
**Episode 9 Inakuja: "MTEGO WA MDOGO WANGU"**