✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 13: USIKU WA DAMU MKANYAGENI

Lailah aliwasili kijijini Mkanyageni usiku wa manane, wakati ambao hata mbwa walikuwa wameacha kubweka kutokana na baridi kali ya ajabu iliyolikumba kijiji hicho tangu alipokanyaga ardhi ya nyumbani. Alikuwa amejifunika kwa khanga mbili kuukuu ili kuficha harufu yake ya mzoga, lakini upepo ulikuwa ukisambaza harufu ile ya ajabu hadi kwenye pua za wanakijiji waliokuwa wamelala.

Alipokaribia nyumba ya mama yake, alimwona mtu ameketi barazani akiwa na tochi na panga mkononi. Alikuwa ni Kelvin. Tangu aliporudi kutoka mjini, Kelvin alikuwa ameapa kumlinda mama Lailah dhidi ya chochote.

"Nimeshakusikia harufu yako, Lailah! Usisogee hatua nyingine!" Kelvin alipiga kelele huku akisimama na kuwasha tochi.

Mwangaza wa tochi ulimulika uso wa Lailah. Kelvin alirudi nyuma kwa mshtuko. Uso wa Lailah ulikuwa umepata makunyanzi, macho yameingia ndani mithili ya fuvu, na sehemu ya kifuani ilikuwa imeloa usaha mweusi uliokuwa ukichuruzika hadi kwenye khanga.

"Kelvin, niondolee hiyo tochi! Nataka kumuona mama yangu," Lailah alizungumza kwa sauti iliyopasuka, sauti ambayo haikuwa ya kibinadamu.

"Humuingii hapa! Wewe ni mchawi, umeleta laana ya mjini hapa kijijini! Mama yako anaumwa kwa sababu ya dhambi zako," Kelvin alijibu huku akishika panga lake kwa nguvu.

Lailah alicheka kicheko cha kikatili. "Dhambi? Mimi natafuta haki yangu! Uzuri wangu umechuchuliwa na hao wazee wenu, na mama ndiye aliyenilaani. Leo nataka kufungua hilo fundo!"

Lailah alichukua ile chupa ndogo aliyopewa na mganga wa Buguruni. Alinywa funda moja na kutema kuelekea kwa Kelvin. Ghafla, moshi mzito wa kijivu ulitanda. Kelvin alihisi miguu yake inakufa ganzi, panga likamdondoka mkononi. Alijaribu kupiga kelele, lakini sauti ilikwama kooni.

Lailah alimpita Kelvin aliyekuwa amepooza, akasukuma mlango wa chumba cha mama yake. Ndani, harufu ya kifo ilikuwa inashindana na harufu ya Lailah. Mama Lailah alikuwa amelala, akivuta pumzi kwa mbali. Alipofungua macho na kumuona Lailah, badala ya kuogopa, alitoa chozi moja la uchungu.

"Mwanangu... umekuja kuniua ili upate uzuri wa duniani?" Mama Lailah alinong'ona.

Lailah hakujibu. Alichukua kisu alichopewa na Sheikh Sharifu. Alisogea kitandani, akamvua mama yake shuka. Mikono ya Lailah ilikuwa inatetemeka, lakini picha ya yeye kuwa mrembo tena na kurudi chuo kutesa ilimpa ujasiri wa kinyama.

Alimshika mama yake koo kwa mkono mmoja, na mkono mwingine ukiinua kisu. "Mama, unisamehe... lakini siwezi kuishi hivi. Nataka 'A' zangu, nataka magari yangu, nataka chuhu zangu zirudi kama zamani!"

Wakati akijiandaa kuchoma kisu kifuani mwa mama yake, ghafla Kelvin, kwa kutumia nguvu za mwisho, alijiburuza na kuingia chumbani huku akipiga kelele ya kuomba msaada. Wanakijiji walianza kuamka.

Lailah alishtuka, akachoma kisu mkononi mwa mama yake badala ya kifuani. Damu nyekundu ilitapakaa. Lailah alichukua kitambaa na kuzoa ile damu ya mama yake kwa haraka, kisha akatoka mbio kupitia dirishani huku akitoweka kwenye giza la msitu wa kijiji, akiacha kilio kikubwa nyuma yake.

Alikuwa amepata damu, lakini hakuua. Je, ile damu kidogo itatosha kumrudishia nyota yake?

---

**Katika Episode inayofuata:**
Lailah anarudi Dar es Salaam na ile damu ya mama yake. Anampelekea mganga, lakini mganga anamwambia damu haijatosha kwa sababu "kafara haijakamilika." Wakati huo huo, Lailah anagundua kuwa chuo kimeanza mchakato wa kumfukuza rasmi. Katika hali ya kuchanyikiwa, Lailah anaanza kuuza damu yake mwenyewe.

**Usikose EPISODE 14: "DAMU ISIYOTOSHA NA KIBALI CHA KUFUKUZWA"**