✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 2: Kuingia Kwenye Kichwa cha Mamba

Happy aliamka asubuhi akiwa anajinyoosha kwa raha, huku akitazama salio lake la simu. Aliona ile elfu thelathini bado ipo, akacheka kwa dharau akimuwaza yule mwanaume aliyemtumia pesa jana yake. “Wanaume kweli ni mazuzu,” aliwaza huku akielekea bafuni.

Wakati anatoka bafuni, alimkuta Asha amekaa mnyonge.
“Vipi shoga mbona umepooza?” Happy alimuuliza.

“Juma anataka nikae kwake wikiendi hii, lakini sina hata nguo mpya ya kuvaa. Naona aibu kwenda vilevile kila siku,” Asha alijibu kwa sauti ya upole.

Happy akacheka, “Shoga yangu, mimi nakwambia kila siku hutaki kunisikia. Tumia ulichonacho upate unachotaka. Angalia hapa,” Happy alimwonyesha Asha ile elfu thelathini. “Hii ni nauli ya jana, na leo nitapata nyingine. Twende sokoni nikakununulie hata kanga mbili mpya.”

Asha akasita, “Lakini Happy, hiyo si hela ya dhuluma? Huyo kaka hajakupigia simu?”

“Anipigie mara ngapi? Nisham-block tangu saa sita usiku. Hawezi kunipata,” Happy alijibu kwa kiburi.

Wakati wanajiandaa kwenda sokoni, ghafla simu ya Happy ikaita. Ilikuwa ni namba ngeni. Happy akaipokea kwa pozi lake la kawaida.

“Halo mrembo,” sauti ya kiume, nzito na ya mamlaka ilisikika upande wa pili. “Nimekuona jana pale karibu na duka la mangi, ukweli nilivutiwa sana na wewe. Naitwa James.”

Happy akageuza macho na kumuashiria Asha kuwa mwingine ameingia kwenye mtego. “Asante James, mimi naitwa Happy. Inakuwaje?”

“Happy, mimi sipendi kupoteza muda. Nataka tuonane leo jioni hotelini kwangu kwa chakula cha usiku. Nitakutumia elfu hamsini sasa hivi, nusu iwe ya taxi na nusu nyingine ukanunue pafyum nzuri unayopenda. Utakuja?”

Macho ya Happy yakazunguka kama feni. “Elfu hamsini? James wewe ni mwanaume wa kweli. Nitakuja, usijali.”

“Sawa, muamala unaingia sasa hivi.” James alikata simu.

Haikupita dakika mbili, ujumbe wa muamala ukaingia. Elfu hamsini! Happy akapiga yowe la furaha na kumkumbatia Asha. “Unaona sasa? Huyu James ni dume haswa. Leo sioni bule, leo nakula kuku kwa mrija!”

Lakini Happy hakujua kuwa James hakuwa mgeni kama alivyodhani. James alikuwa ni kaka wa mmoja wa vijana ambao Happy aliwahi kuwala nauli ya matibabu ya uongo. Na James alikuwa ameshaapa kuwa lazima Happy akomeshe tabia yake hiyo.

James alikuwa ameketi kwenye gari lake jeusi akiwa na vijana wengine wawili. “Ameshaingia kwenye mtego,” James alisema huku akitazama simu yake. “Safari hii hatumtumi elfu kumi kumi, tunamtumia kubwa ili akose ujasiri wa kuizuia namba. Na akifika hapa, atajua kuwa mpenda pumbu, hali nauli kweli.”

Saa kumi na mbili jioni, Happy alijipamba kweli kweli. Alivaa nguo fupi inayobana, akajipulizia pafyum kali na kumuaga Asha. “Shoga yangu, mimi naenda kwa James. Leo sitamzima data huyu, nataka nione ana nini zaidi ya hii elfu hamsini.”

Asha akamtahadharisha, “Happy kuwa makini, mbona unabadilika haraka? Mara umzime, mara uende?”

“Huyu James anaonekana ana pesa, siwezi kumuacha hivi hivi,” Happy alijibu na kupanda taxi iliyokuwa inamsubiri nje.

Taxi ilimpeleka mpaka kwenye hoteli moja kubwa nje ya mji. Happy alishuka kwa maridadi, akajitikisa kidogo na kuelekea mapokezi. Aliambiwa James anamsubiri chumba namba 302.

Alipofika mlangoni, moyo ulimpiga kidogo. Akagonga. Mlango ukafunguliwa na James, akiwa na tabasamu pana. “Karibu Happy, nilijua utakuja.”

Happy akaingia ndani, lakini ghafla alishtuka kumuona mwanaume mwingine amekaa kwenye kochi, na mlango ukafungwa kwa ufunguo kwa nyuma.

“James, huyu ni nani? Na kwanini unafunga mlango?” Happy aliuliza kwa hofu.

James akacheka kicheko cha kikatili. “Huyu ni mdogo wangu uliyemla nauli ya elfu ishirini wiki iliyopita ukasema unaumwa. Na leo, umekula elfu hamsini yangu. Happy, mchezo wa kula nauli umefika mwisho leo.”

Happy akajua sasa ameingia kwenye kichwa cha mamba.

---
**ITAENDELEA...**