โœฆ Matangazo โœฆ

๐Ÿ“– Story Tamu

Episode 9: Nyuma ya Nondo na Machungu ya Selo

Harufu ya choo kilichoziba na unyevunyevu wa selo ndivyo vilivyomkaribisha Happy na Pili Kiswaswadu ndani ya kituo cha polisi. Kwa mara ya kwanza, dharau na maridadi ya Pili yaliisha; alikuwa amekaa sakafuni huku kanga yake ikiwa imejaa vumbi, akilia kwa sauti ya chini. Happy naye alikuwa amejikunyata pembeni, mwili wake ukizidi kumuuma kutokana na kipigo cha hotelini na mishtuko ya kukamatwa.

"Happy, hivi kweli Juma amesema tulikuwa tunajua mambo yake ya wizi?" Pili aliuliza huku akifuta kamasi kwa ncha ya kanga. "Mimi nilijua ana hela za mradi wa ofisini, kumbe anaiba vifaa?"

Happy alimtazama Pili kwa dharau licha ya hali yao mbaya. "Wewe Pili nyamaza. Ulafi wako wa kutaka kuhongwa kila siku ndio umemponza Juma. Na yule mwanaume kwa jinsi alivyobanwa na polisi, ameamua kutuburuza sote ili asife peke yake. Umesikia alivyosema? Kwamba mimi nilikuwa namtishia? Mimi niliula nauli yake mara mbili tu na sikujua hata kama anaiba!"

Wakati wakiendelea kulaumiana, mlango wa selo ulifunguliwa. Askari mmoja alisimama mlangoni na kuita, "Happy! Toka nje, una mgeni."

Happy alinyanyuka kwa matumaini, akidhani labda ni Asha amekuja kumdhamini. Lakini alipofika sebuleni mwa polisi, alimkuta mwanamke mmoja mtu mzima, aliyevalia mavazi ya heshima, akiwa ameketi na Asha. Alikuwa ni mama yake Asha, ambaye alikuwa amekuja mjini kumsalimia mwanawe na kukuta majanga hayo.

"Mama Asha..." Happy alisema kwa sauti ya unyonge, akishindwa hata kuwatazama usoni.

Mama Asha alimtazama Happy kwa masikitiko makubwa. "Happy mwanangu, nimeyasikia yote. Nimekuja hapa kukuona kwa sababu Asha ameniambia jinsi mlivyokuwa mkiishi. Ujana ni maji ya moto mwanangu, lakini ukiyachezea yanakubabua."

Asha alikuwa amekaa kimya, uso wake ukiwa na huzuni lakini haukuwa na hasira tena. Alikuwa amemlipia Happy dhamana baada ya James kukubali kutoa ushahidi kuwa Happy hakuhusika moja kwa moja na mipango ya wizi, bali alikuwa ni "muathirika wa tamaa zake mwenyewe."

"Happy, nimekulipia dhamana," Asha alisema kwa sauti tulivu. "Lakini Pili atabaki hapa kwa sababu amepatikana na baadhi ya vifaa vya ofisi ya James nyumbani kwake. James amesema hatamsamehe Pili hata kidogo."

Happy alianguka miguuni mwa Mama Asha akilia. "Mama nisamehe, Asha nisamehe. Nilijiona mjanja, niliona maisha ni kula nauli na kucheza na hisia za watu. Leo nimepoteza utu wangu, nimepoteza heshima yangu."

Mama Asha alimnyanyua. "Kujuta ni hatua ya kwanza ya kupona. Lakini Happy, mtaa hautosahau haya haraka. Lazima ubadilishe mwenendo wako. Na wewe Asha, mshike mkono rafiki yako, msaidie ajitambue."

Walipotoka nje ya kituo cha polisi, Happy alihisi hewa ya nje ni tofauti kabisa. Alimtazama Asha na kumuuliza, "Juma atafanywa nini?"

Asha alishusha pumzi ndefu. "Juma amepelekwa mahakamani asubuhi hii. James amekataa katakata kufuta kesi. Amesema lazima Juma akae jela miaka kadhaa ili iwe fundisho kwa wafanyakazi wengine na wanaume wanaopenda sifa kwa hela za wizi."

Wakati wakielekea nyumbani, walipita karibu na kijiwe cha vijana. Kelele zilianza upya: "Oya! Mla nauli huyo! Karudi!" Happy alijifunika uso kwa mtandio, safari hii akijua kuwa jina lake limechafuliwa vibaya.

Lakini katikati ya vumbi hilo la aibu, simu ya Asha iliita. Ilikuwa ni namba ya Saidi, boss mkuu wa kampuni aliyokuwa anafanya kazi Jamesโ€”mtu ambaye alikuwa hajawahi kuingilia mambo ya mtaani, lakini safari hii alikuwa na ujumbe mzito kwa ajili ya Asha na mazingira yote yaliyotokea.

---
**ITAENDELEA...**