✦ Matangazo ✦

📖 Story Tamu

Episode 2: DK. 60 ZA JASHO JEMBAMBA

Giza lilizidi kutanda ndani ya sebule yetu, si kwa sababu ya jua kuzama, bali kwa sababu ya hofu iliyoanza kuiteka akili yangu. Nilijaribu kubonyeza kitufe cha *Eject* kwa nguvu, nikiitumaini ile deki ingekuwa na "betri ya akiba" ya kutoa CD, lakini wapi! Ilibaki kimya kama kaburi.

Niliwaza kuibeba deki nzima nikimbilie kwa fundi umeme mtaa wa pili. Lakini nikajifikiria: *"Nikifika kwa fundi, nitamwambiaje? Atoe CD ya ajabu mbele ya wateja wake?"* Hapana, hilo lingekuwa ni kujichimbia kaburi mtaani kote.

Mara, nilisikia vicheko vya washikaji zangu nje. Walikuwa wanakuja.
*"Oyaaa! Vipi, mambo ni moto nini?"* Juma aliniuliza huku akichungulia dirishani.
*"Zima hiyo midomo yenu! Umeme umekata na CD imekwama ndani!"* Niliwanong'oneza kwa sauti ya kukata tamaa.
Badala ya kunionea huruma, wale jamaa walipasuka kwa kicheko. Waliona ni mzaha, lakini kwangu ilikuwa ni hukumu ya kifo.

Muda ukayoyoma mpaka saa kumi na moja jioni. Mara nikamuona mama anakuja kwa mbali akitokea kanisani. Moyo ulitaka kunichomoka kifuani. Mama ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuwasha TV akitaka kusikiliza kwaya wakati akipika.

*"Galous mwanangu, mbona umekaa gizani?"* Mama aliuliza huku akiingia ndani.
Nilijifanya nimejilaza kwenye kochi, nikijifunika shuka mpaka shingoni. *"Mama, nahisi homa kali sana, kichwa kinapasuka,"* nilidanganya kwa sauti ya unyonge.
Mama alinitazama kwa huruma. *"Pole sana, nenda kapumzike. Lakini kabla ya kulala, nenda pale duka la kwa Mangi ukanichukue maziwa ya chai."*

Nilitamani kulia. Nitaendaje duka la mbali wakati umeme unaweza kurudi muda wowote? Nikitoka hapa na umeme ukirudi, mama atawasha TV, na picha za "warumi" zitaanza kucheza mbele ya macho yake matakatifu.

Nilisimama kwa unyonge, macho yangu yakiwa yameganda kwenye ile deki, nikiomba kwa mara ya kwanza maishani mwangu: *"Mungu, naomba umeme usirudi sasa hivi."*

**ITAENDELEA...**

---
**Episode 3 Inakuja: "MTEGO WA TAARIFA YA HABARI SAA MBILI"**