✦ Matangazo ✦

πŸ“– Story Tamu

Episode 6: HARUFU YA HATARI HOSPITALI

Usiku wa pili hospitalini ulikuwa wa baridi na wenye ukimya uliotawaliwa na milio ya mashine na vikohozi vya wagonjwa wengine. Esta alikuwa amejikunyata chini ya shuka, akitazama mwanga hafifu wa mwezi uliokuwa ukipita kwenye dirisha la wodi. Kila mara mlango ulipofunguka, moyo wake ulistuka na kudunda kwa kasi. Alihisi harufu ya Frank kila mahali, harufu ambayo ilishajikita kwenye ubongo wake kama sumu.

Mido alikuwa amekaa kwenye korido, macho yake yakiwa malegevu kwa uchovu lakini akili ikiwa macho. Akiwa kama mpelelezi mwenye uzoefu, alihisi kuna kitu hakiko sawa. Aliona pikipiki moja ikipita mara kwa mara nje ya lango la hospitali, na vijana wawili waliokuwa wamejifunika nyuso zao kwa kofia za koti (hoodies) wakizunguka-zunguka eneo la mapokezi wakijidai kutafuta mgonjwa asiyepo.

"Hawa jamaa wanatafuta kitu," Mido alinong'ona moyoni, huku mkono wake ukigusa bastola yake iliyokuwa kiunoni, imefichwa na shati lake.

Ndani ya wodi, Esta alihisi haja ndogo. Alijaribu kunyanyuka taratibu, akishikilia mirija ya drip. Maumivu yalimchoma kama pasi ya moto, akajikuta akishika chuma cha kitanda kuzuia asidondoke. Ghafla, aliona kivuli kikipita nyuma ya pazia la kitanda chake.

"Nesi?" Esta aliita kwa sauti ya chini, iliyojaa mashaka.

Hakuna jibu. Badala yake, mkono mmoja wenye glavu nyeusi ulisogeza pazia. Esta alitaka kupiga kelele, lakini hofu ilimfunga koo. Alikutana na macho ya baridi ya yule kijana mweusi aliyekuwa na Frankβ€”**Dullah**.

"Ulipaswa kufa kule mtaroni, mdogo wangu," Dullah alinong'ona, akitoa kisu kidogo chenye makali yaliyong'aa kwenye giza. "Sasa unatuingiza gharama za kukufuata hadi hapa."

Dullah alipiga hatua moja kuelekea kitandani. Esta alijisukuma nyuma mpaka akagusa ukuta, akitetemeka na kutoa machozi ya kukata tamaa. Aliona kifo kikimkaribia kwa mara ya pili.

Lakini kabla Dullah hajanyanyua mkono wake, mlango wa wodi ulifunguliwa kwa kishindo kikubwa. Mido aliingia kama upepo wa dhoruba.

"Simama hapo hapo! Polisi!" Mido alipiga kelele, sauti yake ikitetemesha kuta za chumba kile.

Dullah hakusubiri. Aliruka kupitia dirisha la wodi lililokuwa wazi, akatoweka kwenye giza la nje kabla Mido hajafika dirishani kumdhibiti. Mido alitaka kuruka kumfuata, lakini aliposikia sauti ya Esta akianguka chini na kulia kwa nguvu, alighairi. Alirudi haraka na kumnyanyua Esta aliyekuwa amepoteza fahamu nusu kwa mshtuko.

"Esta! Esta, nipo hapa! Usiogope!" Mido alimkumbatia kwa nguvu, akijaribu kumfariji.

Wauguzi walikimbia kuingia ndani, wakishangazwa na ghasia hizo. Mido alikuwa na hasira kali; hakuamini kuwa wahalifu hao walikuwa na ujasiri wa kuingia hadi hospitalini. Alimwangalia Esta aliyekuwa akihangaika kwenye kifua chake, na hapo ndipo Mido alifanya uamuzi mgumu.

"Hapa si salama tena," Mido alimwambia nesi mkuu. "Nanamtoa hapa sasa hivi. Atakaa mahali ambapo nitamulinda mimi mwenyewe usiku na mchana."

Esta alipozinduka kidogo, alijihisi akiwa kwenye kifua kipana cha Mido. Alihisi joto na harufu ya usalama. Kwa mara ya kwanza, hakuona uadui kwa mwanaume huyu. Alijizika kichwa chake kwenye shingo ya Mido, akilia kwa sauti ya unyonge.

Mido alimbeba hadi kwenye gari, akihakikisha amemfunika koti lake. Alijua kuwa kuanzia sasa, amevunja taratibu nyingi za kazi, lakini hakuwa na namna. Moyo wake ulikuwa umeshaungana na binti huyu aliyejeruhiwa, na hakuwa tayari kumpoteza.

---
**Je, Mido anampeleka Esta wapi? Na Frank atafanya nini baada ya Dullah kushindwa kumaliza kazi hospitalini?**

*Usikose Sehemu ya 7: **HIFADHI YA SIRI.***